Hekalu ya Yerusalemu ilikuwa kitovu cha ibada za Uyahudi wakati wa Israeli ya Kale. Kwa jumla kulikuwa na majengo mawili yaliyofuatana kwenye mlima wa hekalu mjini Yerusalemu. Imani ya Kiyahudi inategemea kujengwa kwa hekalu ya tatu pamoja na kuja kwa Masiya wakati ujao.
Katika imani ya Kiyahudi sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ndani ya hekalu ilikuwa mahali ambako Mungu mwenyewe aligusa dunia.
Hekalu ya kwanza ilijengwa na mfalme Suleimani kuanzia mwaka 957 KK. Hekalu hii ilichukua nafasi ya hema ya kukutania iliyotunza vifaa vya ibada za Kiyahudi tangu siku za kale ikaaminiwa tangu Musa.
Hekalu hii ilikuwa mahali pa pekee palipotazamiwa kuwa sehemu halali kwa ibada za sadaka. Hata hivyo kuna taarifa katika Biblia kuhusu ibada kwenye "mahali pa juu" yaani juu ya milima zilizolaumiwa katika Biblia kama ishara ya imani potofu.
Hekalu hii ya Suleimani iliharibika mwaka 587 KK wakati Nebukadreza II wa Babeli alipovamia Yerusalemu na kuharibu mji.
Baada ya ushindi wa Waajemi juu ya Babeli mwaka 539 KK mfalme Koreishi aliwaruhusu Wayahudi kujenga hekalu upya. Kitabu cha Ezra katika Biblia kinasimulia habari hizi.
Ujenzi ulifuata mpango wa hekalu ya kwanza na ulifanya mahali palepale Yerusalemu kwenye "mlima wa hekalu". Katika hekalu hii ya pili sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu ilikaa bila kitu ndani yake kwa sababu Sanduku la Agano lilipotea tangu kubomolewa kwa hekalu ya kwanza.
Hekalu iliharamishwa na mfalme Antiochos IV mwaka 169 KK alipoweka hapa sanamu ya mungu wa Kigiriki Zeus. Hatua hii ilisababisha upinzani wa Wamakabayo waliorudisha ibada ya Kiyahudi hekaluni na hadi leo sherehe ya Hanuka inakumbusha kutakaswa kwa hekalu.
Mnamo mwaka 21 KK mfalme Herode aliamuru matengenezo ya hekalu. Wataalamu wengi huona ya kwamba matengenezo yalifanana na ujenzi mpya hekalu ilipambwa na kuongezeka.
Hekalu inayotajwa katiika taarifa za Agano Jipya ni hekalu hii ya Herode.
Mwaka 70 jeshi la Dola la Roma lilivamia Yerusalemu na kubomoa hekalu. Kuta za msingi zilibaki na ukuta mkubwa wa magharibi unasimama hadi leo ni Ukuta wa Maombolezo wa Wayahudi.
Waroma walijenga hekalu kubwa kwa mungu wao Jupiter iliyobomolewa baada ya ushindi wa Ukristo katika Dola la Roma. Kulikuwa mara mbili na majaribio kujenga hekaluy a Kiyahudi tena matra ya kwanza chini ya Kaisari Julian Apostata na mara ya pili wakati wa uvamizi wa Uajemi kwenye vita dhidi ya Bizanti mnamo 614 lakini majaribio yote yalishindikana.
Waislamu walipovamia Yerusalemu walikuta mlima wa hekalu kama mahali pa maghofu tu wakajenga hapa msikiti. Leo hii kuna majengo ya kiislamu ya msikiti wa Al Aqsa pamoja na Kubba ya Mwamba.
Ukuta wa magharibi wa hekalu ya Herode unaoitwa Ukuta wa Maombolezo ni mahali patakatifu pa Wayahudi.